Saturday, November 26, 2011

MIAKA HAMSINI YA UHURU: MISINGI MIKUU YA MTAZAMO WA MWALIMU JULIUS K. NYERERE KATIKA KUJENGA TAIFA

 
UHURU SONG SPECIAL(BONGO FLAVOR)   

Tanzania Bara inatimiza miaka hamsini ikiwa huru na imetimiza
miaka 47 tangu iungane na Zanzibar na kuunda taifa moja na nchi
moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika matukio hayo
mawili makubwa na muhimu katika uwepo wa Tanzania ya sasa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amekuwa sehemu na kiongozi
wa kupatikana kwa yote hayo. Kwa hali hiyo haiyumkini
kuzungumzia taifa la Tanzania bila ya kumjadili Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.
Katika mada hii nimetakiwa kujadili misingi mikuu ya mtazamo wa
Mwalimu Julius K. Nyerere muasisi wa Taifa huru la Tanzania Bara
na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ujenzi wa
taifa. Muasisi huyo ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere ambaye alikuwa Mwalimu aliyechukua uamuzi mgumu wa
kuacha kazi hiyo na mapato yake na kuwa kiongozi wa chama
kilichoongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanzania Bara
mpaka ukapatikana. Uhuru uliopatikana mwaka 1961 palikuwa na
nchi iliyoitwa Tanganyika sasa Tanzania Bara iliyokua mkusanyiko
wa makabila ambayo mwono wa Kitaifa ulikuwa umefifishwa kwa
makusudi na ukoloni.

Wakati wa machweo ya ukoloni na mapambazuko ya Uhuru hisia
na mtazamo wa utaifa ulisisitizwa na Mwalimu Julius Nyerere
aliyekuwa Waziri Mkuu na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Mwalimu Nyerere aliwekwa kipaumbele mara baada
ya Uhuru wa kujenga taifa moja lililotoka katika mkusanyiko huo
wa makabila yaliyojikita katika misingi maalum aliyoitanabahisha
bila taswishi wala mashaka. Misingi hiyo ni utu, uhuru, usawa na
haki, maendeleo ya watu, kujitegemea, uzalendo, utaifa na
umoja, amani na utulivu, maadili na demokrasia shirikishi. Ni
kwa kuijenga na kuisimamia kwa dhati misingi hiyo ni moja ya
sababu ambayo imemfanya Mwalimu Julius Nyerere kuwa alama
au taswira ya uhuru, uzalendo na utaifa wa Tanzania.
Ingawa katika mada hii msisitizo ni katika misingi mikuu ya
mtazamo wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kujenga
taifa letu la Tanzania naona kuna haja ya kutoa maelezo ya usuli
juu ya Tanzania ni nini na Mwalimu Nyerere ni nani. Naamini hilo
litayaweka maelezo yangu katika muktadha wake. Nikiri kuwa
mimi sijatanabahisha katika Taaluma ya siasa wala katika taaluma
ya uongozi. Hivyo mada yangu inaweza kuwa na upungufu hata
hivyo nafarijika kuwa katika hadhara hii wapo waliobobea katika
hayo na hivyo watafafanua vyema yale yatakayokuwa pogo katika
maendeleo yangu. Tuanze kwa kujadili chimbuko la Tanzania
ambalo limejengwa katika misingi mikuu iliyowekwa chini ya
uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Uwepo na Chimbuko la Taifa la Tanzania
Tanzania ni Taifa linalotambulika na kuheshimiwa duniani lakini
halikuwepo tangu zamani zote. Tanzania katika mipaka ya leo ni
matokeo ya misukumo mbalimbali lakini mikubwa mitatu. Moja
Tanzania ni matokeo ya maumbile ya asili ya kijiografia yenye
mazingira yaliyowafanya watu kutoka sehemu nyingine katika
nyakati mbalimbali kabla ya ukoloni kuja na kuishi katika eneo
ambalo leo ni Tanzania. Kundi kubwa la watu lililokuja miaka
kadhaa kabla ya ujio wa ukoloni wa Kijerumani ni Wangoni. Ni
maumbile hayo ya kijiogafia baadaye yalitumiwa kuwa sehemu ya
mipaka ya nchi iliyowekwa na wakoloni. Mlima Kilimanjaro, Ziwa
Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Mto Ruvuma na Bahari ya
Hindi ni sehemu ya maumbile ya asili yanayoweka mipaka na nchi
nyingine. Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda ,
Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Zambia, Malawi na
Msumbiji.
Msukumo wa pili ulioifanya Tanzania Bara kuwa katika mipaka ya
leo ni historia ya ukoloni wa Kijerumani na mikataba ya kibeberu
iliyowekwa kati ya Wajerumani na Waingereza. Ukoloni ulikuja na
kupora ardhi yetu na kuitawala. Katika eneo hili Wajerumani,
Waingereza na Wabelgiji waligombea maeneo ya kutwaa na
kuyatawala ama kwa hila na ulaghai na hata kwa vita na kwa
kutumia nguvu.
Mipaka hiyo imedumu kwa kiasi kikubwa hata baada ya uhuru na
Mwalimu Julius katika mkutano wa Wakuu wa Nchi wanachama
wa Umoja wa Afrika uliofanyika Cairo, Misri mwaka 1964
aliwasilisha hoja kuwa mipaka iliyoachwa na wakoloni iheshimiwe

ilivyo ili kuepusha vurugu na mifarakano na hata vita kwa mataifa
machanga ya Afrika. Hiyo ilikuwa na mantiki hasa ikizingatiwa
kuwa lengo kubwa la nchi za Afrika lilikuwa bado ni kuunda umoja
wa Afrika.
Mipaka hiyo iliyowekwa na wakoloni ndiyo iliyomfanya Mwalimu
Nyerere alipozaliwa Aprili 1922 azaliwe katika nchi ya Tanganyika
wakati huo katika himaya ya Waingereza kama “mandate territory”
“League of nations”.
Kwa hiyo Tanzania ipo katika mipaka yake ya sasa ikiwa ni
matokeo ya ukoloni wa Wajerumani na hatimaye Waingereza.
Maamuzi ya wakoloni hao juu ya mipaka kama yangebadilika basi
Nyerere asingezaliwa katika eneo ambalo leo ni Tanzania.
Kama ilivyowahi kuelezwa na aliyekuwa Balozi wa Ujerumani
nchini Tanzania, Dr. Heinz Scheneppen katika kitabu kidogo
kiitwacho“Why Kilimanjaro is in Tanzania: Some Reflections
on the Making of the Boundaries” ameandika hivi:
“Was Mwalimu aware that his personal destiny had been shaped by
the borders as well? Had not the Germans in 1886 at the last minute
– as we saw – succeeded in shifting the border east of lake Victoria
by 100 kilometres up to north Musoma, Julius Nyerere would have
not been born in Tanganyika but in Kenya. It would have hardly
been possible for him to become here in Tanzania Baba wa Taifa –
Father of the Nation ….. History in the making, history in the state of
conception has many options; history made, history concluded has no
alternative. Today Tanzania must take the borders as they exist…
Tanzania has developed into a state within the borders imposed by

colonial powers. Within these borders Tanzania has developed into
one nation, overcoming tribal antagonism and ethnic isolation.”1
Dr, Heinz Schneppen anarudia kwa msisitizo juu ya hilo katika
kitabu kidogo kiitwacho “Why Tanzania is Where It Is:
Tanzania’s Colonial Boundaries from the Berlin Conference
1884 – 1885 Until Its Independence”. He observes that:
“Tanzania is where it is because its boundaries are what they
are.That is how we started. No state without boundaries. Without
colonial boundaries there is no Tanzania. But these boundaries,
necessary as they are not at all sufficient condition for Tanzania’s
national existence. A state needed boundaries, but a nation needs a
political will to live together and to belong together. While elsewhere
nations are still searching for their state, in Tanzania the people and
the state have built a nation: within boundaries that are neither
challenged from without nor from within.”2
Kwa hiyo uamuzi wa kuwafanya Wadigo waishi Kaskazini
Mashariki ya Tanzania na wengine wawepo Kenya, Wanyamwanga
wawepo Kusini Magharibi ya Tanzania na
________________________________
1 Schneppen,, H., Why Kilimanjaro is in Tanzania: Some Reflections of This Country and Its Boundaries,
Dar es Salaam, national Museum of Tanzania, Occasional Paper No. 9, 1996,p. 35.
2 Schneppen, H. , Why Tanzania is Where It Is: Tanzania’s Colonial Boundaries from the Berlin
Conference 1884 – 1885 Until Its Independence, Dar es Salaam, National Museum of Tanzania,
Occasional Paper No. 11, 1998, p. 32.

wengine waishi Zambia ni matokeo ya ukoloni. Lakini kwa Wadigo
hao na Wanyamwanga hao leo kuwa watu wa taifa moja na
wanaojivunia utaifa wao mmoja wala sio makabila yao au nasaba
yao ni matokeo ya jitihada madhubuti za Mwalimu Nyerere na
uongozi wa nchi wa kuunda taifa moja. Kama alivyosema Mwalimu
mwenyewe katika hotuba yake aliyoitoa katika Chuo Kikuu cha
Toronto, Kanada tarehe 2 Oktoba 1969 aliyoiita “Stability and
Change in Africa” kwamba:
“In Tanzania it was more than one hundred tribal units which lost
their freedom; it was one nation that regained it.”
Kwa mtazamo wa Mwalimu Afrika haikuwa na chaguo zaidi ya
kuunganisha makabila katika mipaka iliyorithiwa kuwa na haiba
ya taifa.
Kazi ya kuunganisha makabila hayo yote kuwa taifa moja haikuwa
ndogo au rahisi kama inavyodhaniwa na watu wanaopenda kubeza
au kupuuza mafanikio hayo ya Mwalimu. Zipo nchi za Kiafrika
ambazo hadi leo zimebaki kuwa mkusanyiko wa makabila na
mengine yakifarakana na kuhasimiana ndani ya mipaka yao
waliyoirithi kutoka kwa wakoloni. Kama methali ya Kiswahili
inavyosema ukiona vinaelea vimeundwa.

Jitihada hizo za kuunda taifa moja chini ya uongozi wa Mwalimu
Nyerere ndio msukumo wa tatu ulioifanya Tanzania kuwa ilivyo leo
ikiwa ni taifa moja lenye umoja na ni hatua na jitihada za
makusudi zilizochukuliwa mara baada ya uhuru katika ujenzi wa
taifa.
Katika kuunda taifa moja Tanzania imekwenda mbele zaidi. Hii
ndiyo nchi pekee ya Kiafrika ambayo ni matokeo ya muungano wa
hiari wa nchi mbili zilizokuwa huru kuungana kuwa taifa moja.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni matokeo ya muungano wa
iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Muungano ya
Watu wa Zanzibar uliofanyika rasmi tarehe 26 April 1964.
Muungano huo wa kisiasa ambao sasa una umri wa miaka 47 ndio
pekee uliobaki katika Bara la Afrika baada ya mingine kuvunjika
muda mfupi baada ya kuasisiwa. Katika kipindi hicho
kinachoelekea nusu karne muungano huo umepata changamoto
nyingi na hata misukosuko ambayo ingeweza hata kuvunja
muungano wenyewe. Sasa na tuangalie misingi na mitazamo ya
Mwalimu Nyerere aliyoiweka, kuifafanua na kuisimamia katika
ujenzi wa taifa.
3. Mwalimu Nyerere na Misingi ya Ujenzi wa Taifa
Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kama ilivyoelezwa katika sehemu
iliyotangulia ilikuwa kuunda taifa moja kutokana na makabila zaidi
ya 120 aliyoyarithi Tanzania Bara ilipopata uhuru mwaka 1961.
Azma hiyo ilibaki na kupewa msukumo mkubwa zaidi wa kuunda
taifa moja la Watanzania wanaotokana na Muuungano wa
Tanganyika na Zanzibar kuwa wamoja.

Ipo misingi ambayo Mwalimu Nyerere katika mtazamo wake ilikuwa
muhimu katika ujenzi wa taifa. Misingi hiyo ambayo
tumeriorodhesha awali ni utu, uhuru, usawa na haki, maendeleo
ya watu, kujitegemea, uzalendo na utaifa, umoja, amani na
utulivu, maadili na demokrasia shirikishi.
Kwa hiyo ujenzi wa taifa moja la Tanzania si matokeo ya kiajali
wala uholela bali jitihada mahsusi zilizojitika katika misingi hiyo. Ni
misingi hiyo inayowezesha kuundwa kwa taifa moja, imara, lenye
mshikamano na linaloweza kuhimili misukosuko, mikiki mikiki,
vishindo, matatizo na hata husuda na hujuma. Hii ni misingi
inayojenga watu katika taifa lenye msimamo na la watu wazalendo
na wanaojiamini na kuchukua hatua za kulijenga na kuliimarisha
taifa lao.
Msingi wa kwanza wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi wa taifa ni
UTU. Kwamba kila mtu anastahilli heshima kwa sababu ya utu
wake. Utu wa binadamu si kitu cha kupewa kwa ridhaa ya watu
wengine bali ni asili aliyozaliwa nayo mwanadamu. Utu haupewi
kama hisani bali ni haki ya asili ya kila mwanadamu. Kitendo cha
kuwakamata watu na kuwafanya watumwa au kuwatawala na
kuwabagua kinavunja na kutweza utu ambao ni haki ya msingi na
isiyoondosheka ya binadamu. Kwa kutambua umuhimu wa msingi
huo wa utu Chama cha TANU chini ya uongozi wa Mwalimu
Nyerere kilipigania uhuru ili kurejesha utu wa Mtanzania na
baadaye kuwa ndio msingi wa ujenzi wa taifa jipya.

Dhana na msingi wa utu umelezwa na kufafanuliwa na Mwalimu
Nyerere kwa kina katika kitabu chake cha “Binadamu na
Maendeleo” ambacho pia kipo katika kiingereza “Man and
Development” Ni kwa kuamini katika msingi huu kulikomfanya
Mwalimu Nyerere achukie na kukemea kila aina ya ubaguzi ndani
na nje ya mipaka ya Tanzania.
Msingi wa pili katika ujenzi wa taifa letu ni UHURU. Msingi huu
ndio unaoimarisha utu wa mwanadamu. Uhuru katika maana yake
pana mabayo ni zaidi ya kuacha kutawaliwa na taifa jingine bali pia
ni ule uliojengwa katika ukombozi wa mtu na kuboresha maisha
yake na uwezo wake wa kushiriki, kuamua na kusimamia
maendeleo na ustawi wake na wenzake. Katika kusimamia msingi
huu mara baada ya uhuru Mwalimu Nyerere alitangaza vita dhidi
ya adui watatu yaani umaskini, ujinga na maradhi wanaofisha
uhuru wa watu. Jitihada za kupambana na maadui hao watatu ni
sehemu ya hatua muhimu ya ujenzi wa taifa. Mwalimu alitamka
bayana kuwa: “Pasipo huru hakuna maendeleo, na bila
maendeleo uhuru hutoweka.”
Kupambana na maadui hao watatu na madhila mengine lengo lake
ni kuleta maendeleo. Huu ndio msingi wa tatu katika mtazamo wa
Mwalimu Nyerere wa ujenzi wa taifa. Mwalimu Nyerere aliamini na
kusimamia MAENDELEO YA WATU. Kwake lengo la maendeleo ni
watu na hata akatoa hotuba aliyoiita “The Purpose is Man.”

Kitabu cha Tatu cha mkusanyiko wa hotuba na maandiko yake
kiitwacho “Freedom and Development/Uhuru na Maendeleo”
Mwalimu anachanganua na kufafanua dhana na msingi wa
maendeleo ya watu. Ndiyo maana katika moja ya hotuba zake
anasisisitiza kuwa:
“Maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Mabarabara,
majumba kuongeza mazao na vitu vingine vya aina hii, siyo
maendeoeo: ni vyombo vya maendeleo:
Msingi wa nne katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere wa ujenzi wa
taifa ni USAWA NA HAKI. Azma ya kupigania uhuru wa Tanzania
Bara ilikuwa ni kuleta usawa kwa watu. Ndiyo maana ahadi ya
mwana TANU ilikuwa “Binadamu wote ni sawa.” Na usawa
unaandamana na haki ili kukamilika. Usawa na haki ndio
unaimarisha utu wa mwanadamu kwa kuilinda haki yake ya kuishi
katika maana yake pana na haki ya kutoa maoni na kushiriki
katika maamuzi ya umma.
Msingi wa tano katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi
wa taifa ni kujitegemea. Mwalimu alisisitiza umuhimu wa
kujitegemea katika ngazi ya taifa na raia mmoja mmoja. Alitamka
kinagaubaga kuwa Tanzania haina mjomba kwa hiyo ni lazima
ijitegemee na kuleta maendeleo yake. Lakini pia alisisitiza kuwa
taifa omba omba linapoteza uhuru wake na uwezo wake wa
kujiamulia mambo yake.
11
Katika ngazi ya mtu mmoja mmoja Mwalimu Nyerere alikemea
MAKUPE yaani watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini wanaishi
kwa kutegea ndugu zao badala ya kufanya kazi ili wajipatie riziki.
Alitoa kauli mbiu – Usiwe Kupe Jitegemee”. Dhana na msingi
huu umefafanuliwa vizuri na kwa kina katika Azimio la Arusha
lililoleta siasa ya “Ujamaa na Kujitegemea”. Aidha huu
umefafanuliwa vyema na Mwalimu Nyerere katika hotuba na
maandiko yake yaliyokusanywa katika kitabu chake cha pili
kiitwacho “Uhuru na Ujamaa/Freedom and Socialism”. Azimio la
Arusha linatamka kinagaubaga kuwa fedha sio msingi wa
maendeleo bali WATU, ARDHI, SIASA SAFI NA UONGOZI BORA.
Msingi huu wa kujitegemea umeelezwa na Gilbert Rist katika
kitabu chake “The History of Development: From Western
Origins to Global Faith” London,Zed Press, 2008) kuwa ni
chanzo muhimu kwa Mwalimu Nyerere kwa dunia katika
kudadavua matatizo ya kutokuendelea na utegemezi katika mfumo
wa uchumi usio sawa duniani.
Msingi wa sita katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere wa ujenzi wa
taifa unajumuisha dhana za UMOJA, UTAIFA na UZALENDO.
Umoja wa kitaifa ambao ni endelevu unajengwa na mwono wa
utaifa na moyo wa uzalendo. Taifa ambalo halina utaifa na
uzalendo litayumba na kutumbukia katika mifarakano na
kuparaganyika. Uzalendo yaani moyo wa kulipenda taifa ndio
unaofanya watu waweke maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yao
binafsi.
12
Moyo wa kuiona Tanzania ikiwa taifa ni muhimu zaidi kuliko mtu
mmoja mmoja au kundi au kikundi. Uzalendo pia ni moyo wa kuwa
tayari kuitumikia nchi kwa moyo wote. Hapana shaka Mwalimu
Nyerere aliusimamia kidete uzalendo na yeye mwenyewe alikuwa
mfano wa kuishi kwa uzalendo katika uongozi na maisha yake.
Msingi wa nane katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere wa ujenzi wa
taifa ni AMANI na UTULIVU. Amani na utulivu ni tunu ambayo
Mwalimu Nyerere na waasisi wa taifa letu wametuachia. Amani na
utulivu unatokana na taifa kujenga maelewano katika
mazungumzo ya hoja na maelewano katika mambo ya msingi
katika kushughulikia haki za watu na ustawi wao. Ni moyo wa
kuvumiliana na kuheshimiana uliojengwa katika misingi ya haki.
Moyo wa uzalendo huimarisha amani na utulivu kwa kuwezesha
watu kupembua ni mambo yapi ya msingi hivyo yasichezewe na
yapi siyo ya msingi na hivyo yasiruhusiwe kuwa mwanzo wa
mifarakano na utengano na hivyo kudhoofisha taifa.
Msingi wa Tisa katika mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika ujenzi
wa Taifa ni MAADILI. Hapa nina maana ya maadili mema na
maadili ya Ki-Tanzania ambayo pamoja na kuwa ni sehemu ya
jumuiya ya kimataifa Tanzania imejitanabahisha na kujipambanua
kuwa taifa linalosimamia usawa na haki kwa watu wote na mahali
popote.
13
Miongoni mwa misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia kwa
dhati tangu mwanzo wa uhuru wetu miaka 50 iliyopita ni maadili.
Kwa kuzingatia msemo wa Kiswahili samaki mkunje angali mbichi
Mwalimu Nyerere toka awali kabisa alikemea na kuchukua hatua
madhubuti dhidi ya vitendo vya rushwa, udanganyifu, ubadhilifu,
ulaghai, ubaraka, matumizi mabaya ya madaraka,
kutokujiheshimu na kutoheshimu wengine. Misingi hiyo ya
maadili ni muhimu kwa Taifa lenyewe na kwa kila raia.
Umuhimu wa maadili ya kitaifa umeelezwa kwa urefu na kina
katika andiko la Mwalimu Nyerere linaloitwa “National Ethic”.
Msingi wa kumi katika mtazamo wa Mwalimu katika ujenzi wa taifa
ni DEMOKRASIA SHIRIKISHI. Hii ni demokrasia iliyojikita katika
kuhakikisha kuwa wananchi wenyewe ndio waamuzi wa hatima yao
na nchi yao. Ni demokrasia iliyokitika katika siasa za maendeleo na
ustawi wa watu na sio kukimbilia madaraka. Hata alipoelezea
mfumo wa kidemokrasia wa chama kimoja hoja kubwa ilikuwa ni
kuwashirikisha wananchi katika maamuzi. Pia uliporejeshwa
mfumo wa vyama vingi msisitizo wake ulikuwa ni kupanua wigo wa
demokrasia kwa kuwashirikisha zaidi wananchi na kushindanisha
sera kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo na kuimarisha
ustawi wa wananchi.. Umuhimu wa Misingi hii katika Mawanda ya Sasa
Utandawazi pamoja na mabadiliko makubwa ya kisiasa na
kiuchumi unaifanya misingi hii iwe muhimu zaidi sasa katika
kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa taifa moja lenye
kuheshimu utu, linalosimamia usawa na haki, linalojenga
maendeleo ya watu katika misingi ya kujitegemea, linalohimiza
amani na utulivu na lililojikita katika maadili. Katika zama hizi
umoja wa kitaifa hauna budi kusisitizwa na kusimamiwa kwa
dhati kwani kuna kila dalili kuwa vimelea ambavyo vinaweza
kuathiri na kuvuruga umoja wa kitaifa havijatoweka na viashiria
vinaonekana. Ukabila na udini lazima ukemewe kwa nguvu zote.

 Hitimisho

Miaka hamsini baada ya uhuru wetu misingi hiyo bado ni nguzo
muhimu za ujenzi wa taifa letu. Misingi hii daima inasukwa sukwa
na dhoruba ambazo Mwalimu Nyerere amezielezeaa katika hotuba
yake maarufu iitwayo NYUFA” .Hotuba hiyo ni wosia mkubwa kwa
watanzania kwani misingi ambayo tukiichezea na kuipuuza
tunaitakia na tunajitakia maangamizi kama taifa na kama raia wa
nchi hii ambayo kama nilivyoeleza haikujengwa kwa bahati nasibu
au ajali bali kwa mipango na nia madhubuti ya kuwa taifa moja,
huru lililo na usawa na linalosimamia haki kwa ustawi wa watu
wake wote na wale wote wanaotafuta hifadhi katika nchi hii.
Mwalimu Nyerere aliisimamia na kuiishika misingi hiyo, sasa ni
wajibu wetu nasi kuisimamia na kuilinda kwa uwezo wetu wote.
Kama alivyosema yeye mwenyewe Mwalimu Nyerere:
“IT CAN BE DONE PLAY YOUR PART”
“INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO”
                                    Na
Prof. P. J. Kabudi
Kitivo cha Sheria
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Infolinks In Text Ads

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

we gOt friends too